Monday, August 19, 2013

SIRI ZA TRAFIKI FEKI ZAFICHUKA,YADAIWA ALIANZA KAZI MKOANI SINGIDA,AKAJIPA UHAMISHO WA KIKAZI HADI DAR...!!

SIKU chache baada ya kukamatwa kwa askari 'feki' wa Usalama Barabarani mwenye cheo cha Sajini, akifanya kazi ya kuongoza magari eneo ya Tabata Kinyerezi, Dar es Salaam, mambo mapya yamezidi kubainika juu ya sababu za mtu huyo kujiingiza katika kazi hiyo bila kutambuliwa na Jeshi la Polisi.


Habari zilizolifikia gazeti hili kutoka vyanzo vya kuaminika, zinasema trafiki huyo 'feki', ambaye inadaiwa jina lake halisi ni James Juma Hussein (45), mkazi wa Kimara Matangini, alianzia kazi hiyo mkoani Singida kabla ya kujipa uhamisho wa kikazi kwenda Dar es Salaam.

Chanzo chetu kilieleza kuwa, trafiki huyo alikuwa na shemeji yake aliyeitwa Shaban ambaye aliajiriwa na Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani aliyekuwa akifanyia kazi mkoani Tabora.Vyanzo vyetu viliongeza kuwa, baada ya shemeji yake kufariki mkoani Tabora, trafiki huyo alipata mwanya wa kuchukua nguo za kazini alizokuwa akizitumia shemeji yake.



Inadaiwa trafiki huyo 'feki', aliwahi kupata mafunzo ya upolisi katika Chuo cha Polisi Moshi (CCP), mkoani Kilimanjaro lakini alifukuzwa.Chanzo hicho kiliongeza kuwa, baada ya ndugu wa trafiki huyo kufariki dunia, trafiki 'feki', alikuwa akifanya kazi hiyo bila ndugu zake kujua akianzia mkoani Singida bila kushtukiwa.

"Jamaa aliamua kujirithisha kazi ya shemeji yake, alikwenda Singida na kufanya kazi hiyo kwa muda usiojulikana," kilisema chanzo chetu.Chanzo hicho kiliongeza kuwa, kutokana na uchache wa matrafiki mkoani Singida, aliingiwa hofu ya kuweza kujulikana; hivyo aliamua kujipa uhamisho wa kwenda jijini Dar es Salaam.

"Akiwa Dar es Salaam, alifanya kazi hii kwa muda mrefu bila kujulikana hadi alipokamatwa wiki iliyopita akiwa eneo lake la kazi akiongoza magari," kilisema chanzo hicho.Mtoa habari huyo alisema polisi walianza kumtilia shaka trafiki huyo kutokana na adhabu zake alizokuwa akizitoa kwa madereva.

"Tulianza kuwa na hofu naye kwa sababu yeye adhabu zake kwa kila dereva aliyekuwa akimkamata alimtoza sh. 20,000 hadi 25,000," kilieleza chanzo hicho.Sababu nyingine iliyowafanya polisi wamtilie shaka ni utamaduni wake wa kuondoka mapema kwenye kituo cha kazi ambavyo alikuwa akijipangia mwenyewe.

"Trafiki akiwa kazini, inabidi awe kituoni kwake kuanzia asubuhi hadi jioni muda wa kazi unapomalizika, tulishangaa kuona mwenzetu anaingia kazini asubuhi na kuondoka kabla ya muda wa kazi," kiliongeza chanzo hicho.Inadaiwa trafiki huyo alikuwa akifanya hivyo baada ya kukamilisha mahesabu yake aliyokuwa amejiwekea ambapo hali hiyo iliwafanya polisi waanze kujiuliza maswali na ndipo walipoanza kumfuatilia.

Baada ya kufuatiliwa bila yeye kujua, walibaini hata upigaji wake wa saluti ni utata mtupu ambapo kutokana na hali hiyo, waliweka mtego na kufanikiwa kumkamata.
Hadi sasa anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi ambalo limeahidi kutoa taarifa kamili baada ya uchunguzi wao kukamilika

No comments:

Post a Comment