Monday, August 19, 2013

KAMA ULIPANDA MBEGU SHAMBA LA "DECI" UTARUDISHIWA.......




MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imewahukumu kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya sh milioni 21 vigogo wanne wa iliyokuwa Kampuni ya Development Entrepreneurship for  Community Initiative (DECI ).
  Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Alocye Katemana, pamoja na adhabu hiyo pia ameiagiza serikali ifanye mchanganuo wa mali za DECI ambazo inazishikilia, kwa kuwa zipo mali zilishikiliwa zisizo za kampuni hiyo bali za watu wengine.

Alisema kuwa fedha za wateja wa DECI walizopanda zirejeshwe kwa wateja wenyewe ambao wataonesha uthibitisho wa kweli kuwa walipanda fedha zao huko.
 
Katika hukumu hiyo iliyotolewa na Hakimu Mkazi, Stewart Sanga na kusomwa na Hakimu Katemana, washitakiwa walikuwa watano, ambao ni Jackson Mtares, Dominick Kigendi, Timotheo ole Loitginye, Samwel Mtares na Arbogast Kipilimba.
 
Washitakiwa hao walikuwa wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Hudson Ndusyepo na Onesmo Kyauke.
 
Hakimu Katemana alisema washtakiwa hao ambao ni wachungaji wa makanisa ya Pentekoste wametiwa hatiani kuanzia wa kwanza hadi wa nne, isipokuwa mshtakiwa wa tano ndiye ameachiliwa huru baada ya mahakama kumuona hana hatia katika makosa hayo mawili.
 
“Mahakama imeridhika kuwa upande wa Jamhuri uliokuwa unawakilishwa na Wakili wa Serikali, Prosper Mwangamila na Justus Mulokozi, umeweza kuthibitisha kesi yao na kwa maana hiyo mahakama inawatia hatiani washitakiwa hao wannne na kumwachilia huru mshitakiwa mmoja, kwa sababu mashitaka dhidi yake Jamhuri imeshindwa kuyathibitisha,” alisema.
 
Alisema katika kosa la kwanza kila mshitakiwa atapaswa alipe faini ya sh milioni tatu au kwenda jela miaka mitatu, na katika kosa la pili kila mshitakiwa atatakiwa alipe faini ya sh milioni 18 au kwenda jela miaka mitatu na kwamba mshitakiwa atakayeweza kulipa faini ataachiliwa huru.
 
Kabla ya hukumu, Hakimu Katemana, aliwapatia nafasi mawakili wa pande zote mbili kuzungumza chochote, ambapo Wakili wa Serikali, Mwangamila, alieleza kuwa washitakiwa ni wakosaji wa mara ya kwanza na kwamba makosa waliyoyatenda yana madhara katika uchumi wa nchi, hivyo akaomba wapewe adhabu kali.
 
Wakili wa washitakiwa, Ndusyepo, alidai kuwa wateja wake ni mara yao ya kwanza kutenda makosa hayo ambayo waliyatenda wakati wakiwa katika harakati za kuwakwamua waumini wao katika lindi la umaskini.
 
Aliomba mahakama isiwapatie adhabu kali kwani wateja wake hawana uwezo wa kulipa fidia, ikizingatiwa kuwa wengine ni wastaafu na hawana huwezo wa kifedha.
 
Jana saa 7:00 mchana, Wakili Ndusyepo aliliambia gazeti hili kuwa tayari ndugu wa Domick na Mtares walikuwa wakielekea benki na ofisa wa mahakama kwenda kulipa faini ili waweze kukwepa adhabu ya kwenda jela.

Juni 12 mwaka 2009, washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, baada ya vuta nikuvute kati ya viongozi na wanachama wa DECI .

Wakili Mwangamila alidai washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka mawili ambayo ni kuendesha na kusimamia mradi wa upatu kinyume cha kifungu 111A (1,3) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16.
 
Alidai kuwa, kati ya mwaka 2007 na Machi 2009, katika makao makuu ya DECI , yaliyopo Mabibo Mwisho, jijini Dar es Salaam, washitakiwa waliendesha na kusimamia mradi wa upatu katika sehemu tofauti nchini, kwa ahadi ya kuwapa wanachama wao fedha zaidi ambazo katika mazingira ya kibiashara ni kubwa kuliko mradi waliokuwa wakiufanya.
 
Mwangamila alidai kuwa, shitaka la pili ni kupokea amana za umma bila kuwa na leseni, kinyume cha kifungu cha 6 (1,2) cha Sheria ya mabenki na Taasisi za Fedha Na. 5 ya mwaka 2006 na kwamba, washitakiwa wote katika kipindi hicho wakiwa kwenye ofisi zao za DECI , walipokea amana kutoka kwa umma bila leseni.

-Tanzania daima

No comments:

Post a Comment