Monday, August 19, 2013
Mtawa wa kanisa katoliki avamiwa na kujeruhiwa huko zanzibar
MTAWA wa Kanisa Katoliki la Bububu visiwani Zanzibar, Sister Irene Ludovik Mwenda (34), amevamiwa na watu wasiojulikana na kushambuliwa na marungu, hali iliyomsababishia maumivu makali mwilini. Sakata la mtawa huyo lilitokea jana, baada ya kuvamiwa na vijana wapatao kumi, baada ya mtawa huyo kuwa anafuga mbwa ambaye inaelezwa kuwa alikula kuku wa mmoja wa vijana hao.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 11 jioni, jirani na maeneo ya Kanisa la Kigango cha Mtakatifu Thesia Beit –el-rus, katika nyumba wanazoishi watawa wa kanisa hilo.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini na Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mtu huyo aliyepigwa ni mwanamke ambaye ni mtumishi wa Kanisa Katoliki la Bububu, Zanzibar.
Kamanda Mkadam, alisema kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliosababishwa na tuhuma za mbwa wa mtawa huyo kuwa amekula kuku wa kijana huyo, ambapo baada ya majibizano kijana huyo alipata jazba, hali iliyosababisha kumpiga ngumi mtawa huyo.
Kamanda huyo alisema kuwa baada ya kutokea tukio hilo, mtawa huyo alikwenda kufungua jalada la malalamiko katika Kituo kidogo cha Polisi cha Beit-el-rus, kuhusu kupigwa kwake na kijana huyo.
“Tupo tunaendelea na uchunguzi juu ya tukio hili, kwani ni ugomvi wa mitaani unaweza kuleta athari kubwa zaidi, lazima tufanye kazi hii kwa umakini zaidi,” alisema Kamanda Mkadam.
Hata hivyo alisema kuwa Jeshi la Polisi linamshikilia kijana huyo kwa ajili ya mahojiano zaidi, ili kujua sababu za kushambuliwa kwa mtawa huyo ambapo mpaka sasa yupo mikononi mwa polisi.
Alisema baada ya kesi hiyo kufikishwa polisi, wazazi wa kijana huyo walifanya juhudi za kuzungumza na mtawa Irene ili kuweza kufikia maridhiano na kijana huyo na pindi wakishindwa kuelewana, shauri lao litafikishwa mahakamani.
Hata hivyo kutokana na makubaliano hayo, mtawa huyo alikubali kumsamehe kijana huyo, huku polisi ikisema kutokana na sababu za kisheria na usalama, kijana huyo hataachiwa na jalada la kesi limepelekwa katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, ili atoe ushauri kuhusu sakata hilo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment