Hata hivyo, mshukiwa huyu pamoja na picha zake alishaandikwa na gazeti la SANI katika toleo lake la Agosti 7-9, 2013 (toleo la 1042) pamoja na namna alivyosafirisha mzigo pamoja na akina Masogange.
Hii ni taarifa ya gazeti hilo:
Unaweza kukimbia lakini huwezi kujificha. Msemo huu unaonekana kutimia kwa kijana anayedaiwa kuambatana na watuhumiwa wa dawa za kulevya waliokamatwa Julai 5 mwaka huu nchini Afrika Kusini, Agness Gerald 'Masogange' (25) na Melisa Edward (24), kunaswa na gazeti hili.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, wasichana hao, Masogange na Melisa walisafiri ndege moja na kijana anayejulikana kwa jina la Nassoro Mangunga wakitoka Dar es Salaam kwenda Afrika Kusini, wakisafiri na ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA), yenye namba SA 189.
Wakiwa katika ndege hiyo Mangunga, Agness na Melisa walikaa kwenye viti vilivyo jirani kabisa huku Mangunga akiwa katikati yao, kwani Agness alikaa kiti namba 23B, Mangunga alikaa kiti namba 23D na Melisa alikaa kiti namba 23A.
Mangunga ambaye ni rafiki mkubwa wa wanamuziki wa Bongo Flava, Rashidi Abdallah Makwiro 'Chid Benz', Mgaza Pembe 'M2theP' na Albert Keneth Mangweha 'Mangwair', wakati akisafiri na mabinti hao walikuwa na jumla ya mabegi tisa kama kumbukumbu za nyaraka za shirika hilo la ndege zinavyoainisha.
Licha ya nyaraka za kusafirishia mabegi hayo kuonesha jina la Agness Gerald ambaye ni mpenzi wa Mangunga tangu mwanzoni mwa mwaka jana, kuwa ndiye aliyelipia mabegi hayo, ila kwenye sehemu ya anuani ya waraka pepe, imeandikwa Mangunga.
Aidha, mabegi hayo, yalikuwa na kilo 150 za dawa za kulevya lakini kila mmoja alitakiwa kusafiri na kifurushi cha kilo ishirini kama mzigo wa mkononi ambao husafiri bila malipo, hivyo watatu hao kwa pamoja walikuwa na kilo sitini wote kwa pamoja, hivyi kubaki kilo 90 ambazo walizozilipia Dola za Marekani 94 badala ya Dola 450.
Mangunga ambaye licha ya kuishi zaidi nchini Afrika Kusini, lakini pia ni mkazi wa maeneo ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Agness na Melisa, walikamatwa Julai 5, 2013 katika Uwanja wa Ndege wa Oliver Thambo, Afrika Kusini wakiwa na dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 150 aina ya Crystal Methamphetamine zenye thamani ya Sh bilioni 6.8 za Kitanzania, na walipotiwa mbaroni, walikuwa na mabegi sita tu kati ya tisa waliyokuwa nayo wakati wanapanda ndege jijini Dar es Salaam.
Inasemekana mabegi hayo matatu yaliondoka na Mangunga na kutokomea kusikojulikana....
Mpekuzi blog
No comments:
Post a Comment