Monday, August 12, 2013
UTAMJUAJE MWENYE MAPENZI YA KWELI?????
Nimeandika mada hii kutokana na watu wengi kushindwa kutofautisha kupendwa kweli na kutamaniwa. Wapo walioingia mkenge kwa neno hilo hasa walio wageni katika uwanja huu wa mahaba. Ukiambiwa unapendwa basi unachanganyikiwa na kusahau maneno matupu hayajengi nyumba.
Nina maana gani?
Watu wengi wamekuwa wakitumia neno hili kama mtego wa kumpata mtu, kwa kujifanya anakupenda sana na nahau nyingi za mapenzi ambazo zinaweza kukufanya masikio yako yazibe na kuona nani kama wewe.
Siku zote mtafutaji ana lugha tamu ya mapenzi na kabla ya kutamka lolote lazima atangulize nakupenda sana na kuongezea ajuavyo. Hii si mara moja watu kuingia mkenge inapotokea wanakutana na hali hiyo.
Lazima uelewe serikali ya mwili wako inakutegemea wewe, ukiipeleka vibaya lawama zitakuwa juu yako. Usiwe na papara ya kutoa uamuzi wa kukubali uambiwavyo unapendwa bila kufikiria kwa kina. Hakuna hata siku moja mtu anayekutaka kimapenzi akuambie anakuchukia.
Fikiri kabla ya kutenda na kuona kauli uliyopewa ina nia gani na wewe, kweli anakupenda au anataka kukuchezea na kukuacha.
Katika uchunguzi wangu nimegundua wengi hupima kwa masikio juu ya kile aambiwacho na si kufikiria nini hasa kilichomvutia aliyekutamkia maneno hayo. Japo kakutamkia anakupenda, ni vema ukafanya kadiri uwezavyo kupata muda kufikiria kwa kina kabla ya kutoa uamuzi wowote ambao unaweza kukufanya uwe na faida au hasara.
Neno nakupenda siyo mapenzi kamili, bali tabia ya mtu na kuonyesha kweli anakupenda kwa dhati. Akupendaye huwa hana haraka ya kufanya ngono, hufuata taratibu zote ili mradi kujenga uaminifu moyoni mwako.
Hii hutokana na kuwa na uhakika wewe ni wake, hana hofu ya kutanguliza ngono mbele katika uhusiano wenu wa kimapenzi. Ukiona umekutana na mtu anayetanguliza ngono baada ya neno nakupenda huyo hakupendi bali anakutamani.
Tumekuwa tunatumia neno nakupenda kama kiwakilishi cha ujumbe wa mapenzi na si penzi kamili.
Mapenzi ya kweli ni ya vitendo na si maneno, anayekupenda utamjua tu wala hajifichi. Atakuwa mpole, mwenye huruma, anayekujali, muaminifu na mtu aliye muwazi mwenye kukupa uhuru wa kumjua kwa undani ili kukuondoa wasiwasi.
Mapenzi mengi ya siku hizi yamekuwa ya usiri mkubwa yenye mipaka. Kama kweli anakupenda kwa nini akudanganye na akuwekee mipaka ya kumjua? Wakati huo mdomoni kwake ana kila nahau tamu za kimapenzi na kulitamka neno nakupenda kama kiwakilishi.
Huyo si mkweli wala hana mapenzi bali ni muongo aliyejificha nyuma ya neno nakupenda. Kuwa macho na watu hawa sipendi kesho uniulize swali hili.source ya mada hii,Muandishi Joseph shaluwa
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment