KWA mara ya kwanza tangu lilipoibuka sakata la watu maarufu kujihusisha
ama na utumiaji au usafirishaji wa dawa za kulevya, jina la mwanamuziki
anayeaminika kuwa na ukwasi mkubwa kwa sasa hapa nchini, Nasseeb
Abdulmaliki, maarufu zaidi kwa jina la Diamond, limeanza kutajwa kuwa ni
miongoni mwa vigogo wa ‘unga.’
Tayari mjadala mkubwa wa chini
chini umeibuka kwa watu mbalimbali wakiwemo mashabiki wake, na taarifa
ambazo zimelifikia MTANZANIA Jumatano kutoka vyanzo mbalimbali zimedai
kuwa, mwenendo wa maisha ya Diamond sasa unachunguzwa na baadhi ya
maofisa wa vyombo vya dola vya ulinzi na usalama.
Kutajwa kwa
jina la Diamond katika sakata hili, kunatiwa nguvu zaidi na mwenendo
binafsi wa maisha wa msanii huyo maarufu wa muziki wa kizazi kipya,
unaokwenda sambamba na ukwasi mkubwa alioupata katika kipindi kifupi.
Kama hiyo haitoshi, safari za nje ya nchi za mwanamuziki huyo
unaohusisha ziara zake nchini Afrika Kusini na Uingereza, pia ni mambo
ambayo yamechochea wingu la mashaka lililofikia hatua ya jina lake
kuingizwa katika mtandao huo ambao katika siku za karibuni, umewagusa
pia baadhi ya watu wenye majina makubwa katika jamii.
Kuhusu
ziara hizo, kilicholeta mshtuko na dukuduku dhidi yake ni kuwapo kwa
taarifa kwamba, katika moja ya ziara hizo za nje ya nchi, Diamond
alifikia hatua ya kusafiri akitumia chumba kinachotumiwa na wageni
mashuhuri (VIP), badala ya njia ya wasafiri wa kawaida.
Mbali na
hilo, taarifa nyingine zinaeleza kwamba, mizigo ya msanii huyo ambaye
mara kadhaa amekuwa akisafiri na kundi la wacheza shoo wake, imekuwa
ikipita pasipo kupitishwa katika hatua za ukaguzi kwa namna ile ile
ilivyokuwa kwa mabinti wawili wa Kitanzania walionaswa nchini Afrika
Kusini baada ya kuruka mfumo wa ukaguzi wa JNIA.
Aidha, ukaribu
wa kimahusiano kati ya Diamond na baadhi ya Watanzania wanaoishi nchini
Afrika Kusini na ambao majina yao pia yameanza kuhusishwa na biashara
hiyo ya mihadarati, ni jambo jingine ambalo limechochea harakati za
kufuatiliwa kwa karibu kwa nyendo za Diamond.
Taarifa zaidi
kutoka JNIA zinaeleza kwamba, miongoni mwa watu wanaoweza wakawa
wamemponza Diamond ni wale ambao walionekana kuwa karibu na Agness
Gerald ‘Masogange’ (25) na Melisa Edward (24), siku walipokuwa
wakisafiri kwenda Afrika Kusini kabla hawajanaswa katika uwanja wa Ndege
wa Oliver Thambo jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini, wakiwa na
shehena ya dawa za kulevya.
Mwenendo wa watu hao unatiliwa shaka
kuwa huenda ni miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya
wenye maskani yao nchini Afrika Kusini, kwa sababu mbali na ukaribu na
wasichana hao, pia walihusika kwa karibu kuusafirisha mwili wa
mwanamuziki Albert Mangwair, aliyefia huko huko Afrika Kusini ambaye
taarifa za kufa kwake ziligumbikwa na matumizi ya dawa za kulevya.
Alipoulizwa
jana na MTANZANIA Jumatano kupitia simu yake ya kiganjani kuhusu
taarifa hizo na iwapo amekwishahojiwa na vyombo vya dola baada ya jina
lake kuanza kutajwa kuwa miongoni mwa orodha ya wasanii wa muziki
wanaosafirisha dawa za kulevya, Diamond alikiri kuwa na pesa za kutosha
kuishi maisha anayoyataka, lakini akakana kujihusisha na biashara hiyo.
Akifafanua
tuhuma moja baada ya nyingine kwa mpangilio aliokuwa akiulizwa na
gazeti hili, Diamond alisema katika maisha yake, hajawahi kujihusisha na
utumiaji au usafirishaji dawa za kulevya, lakini madai hayo yamekuwa
yakitolewa dhidi yake na watu ambao hawajui siri ya mafanikio yake.
“Kazi
ngumu siku zote inalipa, sasa napata matunda ambayo yanatokana na kile
nilichokifanya, iweje watu wanitilie mashaka, Watanzania ni mashahidi
wangu wananiona navyochumia juani, nitaendelea kulia kivulini tu kwani
nakula kwa jasho langu.
“Siyo kweli kwamba mizigo yangu
haikukaguliwa na kama haikukaguliwa na ingekuwa na kasoro, basi
Uingereza wangenitia hatiani, nilipita na nilikaguliwa.” Alisema
Diamond.
Alipoulizwa kuhusu taarifa za kuwa mwanamtandao wa kundi
la Masogange, pia alikanusha kwa kueleza kuwa hata siku aliyosafiri
kwenda Afrika Kusini alikwenda peke yake uwanja wa ndege na kuongeza
kuwa alikwenda huko kwa shughuli za kimuziki, ambapo safari nzima
iligharimu zaidi ya Dola 30,000 za Kimarekani.
“Afrika Kusini
nimekwenda kufanya kazi zangu na safari hiyo imenigharimu zaidi ya Dola
30,000, nilikwenda kurekodi nyimbo yangu mpya inayoitwa namba moja
ambayo itaanza kusikika hivi karibuni.
“Unajua Watanzania sasa
hivi wanajua mtu hawezi kufanikiwa au kupata maendeleo bila kuuza
‘unga’, hili si sawa juhudi za mtu ndizo zinamfikisha alipo, na mimi
juhudi zangu ndio zinanifikisha hapa, watu waache kunijadili vibaya.”
Alisema Diamond.
Kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja ikiwa ni
takribani miezi miwili sasa tangu Watanzania wawili, Agness Gerald
‘Masogange’ (25) na Melisa Edward (24), waliokuwa na uhusiano wa karibu
na baadhi ya wanamuziki maarufu hapa nchini, kukamatwa nchini Afrika
Kusini wakiwa na dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine zenye
thamani ya Sh bilioni 6.8.
Mbali na kuwa na uhusiano wa karibu na
wanamuziki, Edward anadaiwa kuwa alikuwa mfanyakazi katika mgahawa
mmoja maarufu jijini Dar es Salaam, unaomilikiwa na mmoja wa vijana
matajiri hapa nchini ambaye hata hivyo gazeti hili halijafanikiwa
kumpata ili kufanya naye mahojiano.
Wakati huo huo, tayari hatua
za kinidhamu zimekwishaanza kuchukuliwa dhidi ya wafanyakazi wa JNIA
waliohusika kupitisha kilo 150 za dawa za kulevya, ambao Waziri wa
Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ametaja majina yao hivi karibuni na
kuonyesha kwa waandishi wa habari ushahidi wa kuhusika kwao.
-Mtanzania
No comments:
Post a Comment