Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi amesema baadhi ya majina ya
wabunge yametajwa miongoni mwa watu wanaoshukiwa kujihusisha na biashara
ya dawa za kulevya lakini Serikali haiwezi kuwataja hadharani kwa
haraka.
Majibu hayo ya Waziri Lukuvi yamekuja baada ya
wabunge kumbana na wengine wakizomea baada ya kueleza ugumu wa kutaja
majina ya washukiwa pasi na ushahidi wa kutosha.
“Serikali haiwezi kutaja majina haraka kiasi hicho
kwani inaogopa kukurupuka na kushindwa mahakamani, hivyo lazima tuwe
makini sana na jambo hilo. Hatuwezi kukurupuka tu eti ni fulani wakati
hatuna vithibitisho.
“Kumbukeni wengine mpo humu ndani ya Bunge na
tukianza wengi mtakwisha maana katika orodha hiyo kubwa na ninyi mmo na
orodha ni kubwa kweli ambayo wakati mwingine inatakiwa umakini wa hali
ya juu,” alisema Lukuvi alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa
Karatu (Chadema), Mchungaji Israel Natse.
Katika swali lake ambalo lilisababisha kelele za
kuzomea, Natse alitaka majina hayo yatajwe hadharani. Hata hivyo, hali
ilitulia baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuingilia kati na kusema:
“Hii tabia ya zomeazomea siitaki humu ndani, acheni tabia hiyo lazima
mumsikilize mtu kwa kile anachokisema kwanza lakini mtindo huu si
mzuri...”
Patashika hiyo ilitokana na swali la Mbunge wa
Viti Maalumu (CCM), Catherine Magige aliyetaka kujua iwapo Serikali
inaweza kuwaambia Watanzania ukubwa wa biashara hiyo nchini na kama
haioni kama kuna tatizo katika ukaguzi wa abiria na mizigo katika
viwanja vya ndege na juhudi za Serikali kumaliza tatizo hilo.
Akijibu swali hilo, Lukuvi alisema ukubwa wa
biashara hiyo hapa nchini unadhihirishwa na idadi ya Watanzania 274
waliokamatwa kati ya mwaka 2008 hadi Julai mwaka huu kwa kosa la
kujihusisha na dawa za kulevya katika nchi mbalimbali za nje.
Alisema Serikali inafahamu ukubwa wa tatizo la
matumizi ya biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya nchini na alitaja
takwimu za ukamataji wa dawa hizo katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000
hadi Machi, 2012.
Alisema pamoja na kukamatwa kwa Watanzania hao nje
ya nchi, wageni 31 wanashikiliwa mahabusu katika Magereza ya Keko na
Ukonga, Dar es Salaam ambao ni raia wa Iran, Pakistan, Senegal na Afrika
Kusini.
Hata hivyo, katika swali lake la nyongeza, Magige
alisema uteketezaji wa dawa zinazotajwa kukamatwa umekuwa wa siri kiasi
cha kutiliwa shaka kuwa huenda zinachukuliwa na maofisa waliozikamata
ndiyo maana hakuna uwazi.
Kuhusu hilo, Waziri Lukuvi alisema suala la
uteketezaji wa dawa hizo hauko wazi kutokana na sheria zilizopo kutotoa
nafasi ya kuteketezwa mapema kwa kuwa zinatumika kwa ajili ya ushahidi
akisema wakati mwingine hukaa zaidi ya miaka 10.