MAUAJI ya wafanyabiashara wakubwa ‘mabilionea’ yameshika kasi nchini
ambapo baada ya tajiri mkubwa Arusha, Erasto Msuya kuuawa kwa risasi
hivi karibuni, Agosti 3, 2013 bilionea Elia Daniel Endeni (49) naye
aliuawa kwa kupigwa risasi nje kwa mwanamke anayedaiwa kuwa ni mke wake
mdogo aitwaye Juliana Labson (28).
Tukio hilo lilijiri siku hiyo saa 2 usiku maeneo ya Temeke Mikoroshini jijini Dar es Salaam ambako ni nyumbani kwa Juliana.
Elia
alikuwa na kampuni iitwayo Elia Herdons Ltd ya kupakua na kupakia
mizigo ya makontena bandarini, maduka na majumba ambapo polisi walikuta
shilingi 151,000,000 taslimu ofisini kwake akiwa amezihifadhi.
Ilidaiwa
kuwa muda huo, Elia alikuwa amefika nyumbani kwa mwanamke huyo lakini
kabla hajashuka katika gari lake, Pick-up lenye namba za usajili T 319
AFJ alichomolewa kwenye gari na kupigwa risasi na watu wawili
wasiojulikana.
Taarifa zilieleza kwamba waliotekeleza unyama huo walikuwa wakimfuata marehemu huyo kwa nyuma wakiwa kwenye pikipiki.
Baadhi
ya watu waliozungumza na gazeti hili walisema marehemu alikuwa na
kawaida ya kufika nyumbani kwa Juliana nyakati za usiku na kabla ya
kushuka kwenye gari, alikuwa akimpigia simu mwanamke huyo ili afungue
mlango.
“Ilikuwa wakati anapiga simu ndipo alivamiwa na watu hao
ambao walivunja kioo cha gari kwa kutumia kitako cha bastola kisha kutoa
‘loki’ ya mlango na kumchomoa.
“Walimdhibiti bila kutoa sauti,
wakati huo sisi tulikuwa tumekaa nje tukishuhudia lakini tuliamini
kwamba huenda walikuwa wamegongana barabarani kwani hata marehemu
hakusikika akiomba msaada,” alisema mwanamke mmoja jirani ambaye
hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Mwanamke huyo aliendelea kusema kwamba hakukusikika mlio wa risasi, bali marehemu alianza kulia ghafla akiomba msaada.
Aliongeza
kuwa watu walipokaribia eneo la tukio, wauaji hao walipiga risasi
mfululizo hewani, kitendo kilichowafanya watawanyike kuokoa maisha yao
na majambazi hayo yakatoweka.
Inadaiwa majirani walipofika, walimkuta
tajiri huyo akiwa amelala katika dimbwi la damu huku ameishiwa nguvu
kiasi kwamba alishindwa kuongea chochote.
Habari zinasema mke huyo
mdogo aliyezaa naye watoto wawili, alipotoka ndani alizimia baada ya
kuona Elia akiwa katika dimbwi la damu.
Muda mfupi baadaye, polisi
walifika eneo la tukio na kumchukua majeruhi kumpeleka Hospitali ya
Temeke ambapo alifariki dunia akiwa njiani.
Taarifa zinadai kwamba
Julai 28, mwaka huu marehemu Elia alikoswa na risasi akiwa njiani kwenye
gari akitokea msibani Same, Kilimanjaro.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi
Temeke, ACP Engelbert Kiondo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na
kusema kwamba walifika katika eneo hilo wakiwa na wasiwasi kwamba huenda
watu hao walimnyang’anya bastola.
“Ilitubidi twende ofisini kwake
Kurasini na kupekua, tukaikuta bastola. Hili suala linaonekana ni kisasi
kwa sababu wamemuua bila kuchukua kitu chochote, tunaendelea na
upelelezi,” alisema Kamanda Kiondo.
Mazishi ya Elia yalifanyika
Jumatano iliyopita, Same ambapo Juliana alikuwa miongoni mwa
waombolezaji. Mke mkubwa wa marehemu aishiye Kimara King’ong’o jijini
Dar ndiye aliyekuwa ameongoza msiba huo.
No comments:
Post a Comment