Saturday, August 10, 2013

SHEIKH APIGWA PANGA SWALA YA IDD



na Ibrahim Yassin

 SHEIKH Mkuu wa Wilaya ya Kyela, mkoani Mbeya Nuhu Mwafilango, ameshambuliwa na kujeruhiwa kwa panga baada ya kuzuka kwa vurugu katika msikiti mkuu wa wilaya ya Kyela. Vurugu hizo zilisababisha kujeruhiwa vibaya kwa watu wengine watatu baada ya kushambuliwa kwa mapanga na visu.

 Mashuhuda wa tukio hilo wameiambia Tanzania Daima kuwa vurugu hizo zinazoaminika kuwa ni za kugombea madaraka, zilizuka majira ya saa mbili asubuhi jana wakati sheikh huyo akiongoza ibada ya Idd el Fitri katika msikiti huo. Imedaiwa kuwa kundi la vijana likiongozwa na mwanafunzi mmoja wa shule ya sekondari ya kutwa ya Kyela (jina limehifadhiwa) alimshambulia kiongozi huyo kwa panga na kusababisha vurugu kubwa.

 Imeelezwa kuwa kikundi hicho cha vijana ambao baadhi yao wanadaiwa kukodiwa kutoka katika misikiti ya mikoa jirani, wakiwa na mapanga, nondo na visu walianza mashambulizi hayo, na ndipo wakakumbana na hasira za waumini wengine waliokuwa wamejiandaa kukabiliana na mashambulizi hayo. Mmoja wa vijana waliojeruhiwa vibaya kichwani ametajwa kwa jina la Hamis Hussein ambaye alipambana na vijana walioanza kumshambulia sheikh huyo. Imedaiwa kuwa kulikuwa na fununu za kuzuka kwa mapigano hayo, hatua iliyofanya uongozi wa msikiti kutoa taarifa polisi ambao walijipenyeza katika swala hiyo ya Idd.

 Wengine waliojeruhiwa vibaya ni mmoja aliyetajwa kwa jina la Magogo anayetuhumiwa kuchochea vurugu na mapigano hayo katika kile kilichoelezwa jitihada za kuwaondoa viongozi walioko msikitini na kuwadhamini vijana ambao wanadaiwa kuwa ni waasi wa msikiti huo.

Akizungumza na Tanzania Daima Mwenyekiti wa BAKWATA Wilaya ya Kyela Daud Mwenda alisema kuwa kikundi hicho kinapingana na uongozi uliopo msikitini hapo hivyo wanataka kushinikiza waumini wengine waupindue uongozi uliopo. Mganga wa zamu katika Hospitali ya Wilaya ya Kyela ambaye hakutaka kutaja jina lake alikiri kupokea majeruhi watatu waliotokana na vurugu hizo. Kwa upande wake Afisa Tarafa ya Unyakyusa Helly William alisema kuwa ofisi yake imepokea taarifa za vurugu katika msikiti huo na kudai kuwa jambo hilo limewasikitisha sana kama viongozi wa serikali.

William alisema msikitini sio mahali pa kufanyia vurugu bali eneo takatifu linalotumiwa na watu kumuabudu Mungu.
RESPECT TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment